Aokolewa tumboni mwa mama aliyekufa kwa shambulio

0
192

Sabreen alikuwa amekufa kabla ya kumtazama machoni mwanawe. Mama huyo mwenye umri mdogo alikuwa na mimba ya miezi saba na nusu.

Zilikuwa siku zenye hofu ya kila mara, lakini Sabreen alitumaini kwamba bahati ya familia hiyo ingedumu hadi vita viishe.

Bahati hiyo ilitoweka kutokana na kishindo na moto wa mlipuko saa moja kabla ya saa sita usiku wa Aprili, 20, usiku ambao huku Tanzania, Yanga walikuwa wanasherehekea kuwafunga watani wao, Simba 2-1.

Waisraeli walirusha bomu kwenye nyumba ya familia ya al-Sakani huko Rafah ambapo Sabreen, pamoja na mumewe na binti mwingine wa wanandoa hao, Malak wa miaka mitatu – walikuwa wamelala.

Sabreen alipata majeraha makubwa na mumewe na Malak waliuawa, lakini mtoto alikuwa bado hai tumboni mwa mamake wakati waokoaji walipofika eneo hilo.

Walimkimbiza Sabreen hospitalini, ambapo madaktari walimfanyia upasuaji wa dharura ili kutoa mtoto.

Sabreen hakuweza kuokolewa lakini madaktari walifanya kazi ya kumfufua mtoto, wakigonga kifua chake taratibu ili kuamsha hali ya kupumua.

Hewa ilisukumwa kwenye mapafu yake. “Alizaliwa katika hali mbaya ya kupumua lakini anaendelea vizuri,” Dkt Mohammed Salama, mkuu wa kitengo cha dharura cha watoto wachanga katika Hospitali ya Emirati ulioko, Rafah, Kusini mwa Ghaza amesema.