Hali ya afya ya mtoto mchanga wa kike aliyeokolewa kutoka kwenye kifusi cha jengo lililoporomoka nchini Syria, kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea siku ya Jumatatu inaendelea vizuri.
Mama wa kichanga hicho anadhaniwa kuwa huenda alijifungua muda mfupi baada ya kutokea kwa tetemeko hilo na baada ya kujifungua alifariki dunia.
Watu waliomuokoa mtoto huyo wamesema walisikia sauti na walipoendelea kuchimba ndipo walimkuta mtoto huyo huku kitovu chake kikiwa bado kimeungana na cha mama yake.
Baba wa kichanga hicho, ndugu zake wengine wanne wa kuzaliwa naye, nao wamefariki dunia katika tetemeko hilo.
Jengo ilimokuwa ikiishi familia ya mtoto huyo ni miongoni mwa majengo 50 yaliyoharibiwa kabisa na tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha matetemeko.
Picha za kichanga hicho zimesambaa katika vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo ile inayomuonesha mwanaume mmoja akiwa amembeba mtoto huyo huku akiwa ana vumbi mwili mzima.
Takribani watu elfu nane wamefariki dunia katika tetemeko la ardhi katika nchi za Syria na Uturuki.