Afrika Kusini yaomba msaada kufuatia mafuriko

0
302

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amewaomba watu wanaoweza kutoa msaada kwa waathirika wa mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo Jumatatu wiki hii na kusababisha vifo vya watu 60, kutoa msaada wa haraka.

Rais Ramaphosa amesema kuwa serikali yake itatoa misaada inayowezekana kuwasaidia waathirika kama walivyokuwa wameomba, baada ya kuwatembelea watu hao, lakini pia akaomba wale wote wanaoweza kusaidia kufanya hivyo.

Jana serikali ya Afrika Kusini iliwaomba watu wanaoweza kuwahifadhi waathirika wa mafuriko hayo kwenye nyumba zao kuwakaribisha, kwani vituo vilivyokuwa vimetengwa kwa ajili ya watu hao vimelemewa na idadi kubwa ya watu.

Zoezi la uokoaji katika miji ya Durban na Kwazul Natal iliyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo nchini humo linaendelea vizuri,  baada ya maji kuanza kupungua katika baadhi ya maeneo.

Hata hivyo mafuriko hayo yaliyokuwa yakiambatana na maporomoko ya udongo yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu huku baadhi ya vijiji vikiwa vimefunikwa na maji.