Watu takribani 93 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 140 wamejeruhiwa baada ya watu wenye silaha za moto kufyatua risasi katika tamasha la muziki wa rock kwenye ukumbi wa Crocus, nje kidogo ya Jiji la Moscow usiku wa kuamkia leo, mamlaka nchini humo zimesema.
Moto mkubwa ulilipuka katika jengo na kusababisha sehemu ya paa jirani na eneo la kuchezea muziki kuporomoka na taarifa za karibuni zinasema moto huo umezimwa.
Kundi la Islamic State limedai kufanya shambulio hilo, na taarifa zinasema kwamba waliofanya shambulio walikimbia.
Marekani imesema hakuna sababu ya kutilia shaka madai hayo ya Islamic State, Ikulu ya White House ikisema mapema mwezi huu iliionya Urusi kuhusu uwezekano wa kutokea shambulio kwenye “mikusanyiko mikubwa” jijini Moscow.
Urusi bado haijatoa tamko lolote.
Ukraine, ambayo kwa sasa ipo vitani na Urusi, imekana kuhusika kwa namna yoyote.
Picha ya video ambayo BBC imeipata inaonesha washambuliaji wakifyatua risasi ovyo dhidi ya raia waliokuwa wakipiga kelele huku wakijaribu kukimbia na huku milipuko mingi ikisikika.
Habari za karibuni zinaonesha kwamba watuhumiwa wanne wamekamatwa.