Takriban watu 64 wameuawa katika ghasia za kikabila zilizoibuka katika eneo la Nyanda za Juu, Kaskazini mwa Papua New Guinea, vyombo vya habari vimeripoti.
Afisa mmoja wa polisi ameyaelezea mauaji hayo kama “makubwa zaidi” katika historia ya hivi karibuni ya taifa hilo la Pasifiki.
Gazeti la Post-Courier, likinukuu polisi wa eneo hilo, limesema mauaji hayo yalianza alfajiri jana Jumapili katika Wilaya ya Wapenamanda, Mkoa wa Enga.
Limesema yamehusisha makabila yanayohasimiana ya Ambulin na Sikin pamoja na washirika wao.
Polisi wameiambia Post-Courier kwamba wamepata miili 64 kando ya barabara, kwenye nyasi na katika vilima vya Wapenamanda hadi kufikia leo asubuhi.
Gazeti hilo limesema kwamba katika mapigano hayo makundi hasimu yalitumia silaha ‘nzito’ kama vile bunduki za AK47 na M4 na kuongeza kwamba Idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.
Shirika la Utangazaji la Australia (ABC) limesema kwamba ghasia hizo zimehusisha makabila yaleyale ambayo yalihusika na mapigano yaliyoua watu 60 katika Jimbo la Enga mwaka jana.