Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo amekagua maandalizi ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Cuba na ukumbi utakaofanyika Kongamano la Kimataifa la Kiswahili.
Akiwa na mwenyeji wake, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humprey Polepole, Waziri Kombo ameoneshwa ukumbi unaokwenda kubeba watu 400 utakaoendesha kongamano hilo ambao pia utatoa huduma ya lugha tatu; Kiswahili, Kiingereza na Kispanyola.
Waziri Kombo akiwa na timu yake, ameeleza kuridhishwa na maandalizi yaliyofanyika na kumpongeza Balozi Polepole kwa jitihada za maandalizi ya kongamano hilo la kimataifa.
Kongamano la Kimataifa la Kiswahili mwaka 2024 linatarajiwa kufanyika jijini Havana, Cuba, kuanzia Novemba 7 hadi 10. Tukio hili ambalo Rais Samia atakuwa mgeni rasmi linawaleta pamoja wataalamu, wanafunzi, na wadau wa Kiswahili kutoka kote ulimwenguni kwa mijadala, warsha, na shughuli za kitamaduni zinazolenga kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili.