Mwanamuziki wa kizazi kipya cha Bongo Fleva Zuhura Othman maarufu Zuchu amesema tuzo ya AFRIMMA ya Mwanamuziki Bora Chipukizi Afrika aliyoshinda ni kielelezo tosha kwamba muziki wake unatazamwa ulimwenguni hivyo amewaomba Watanzania kuendelea kumuunga mkono katika kazi zake.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwanamuziki huyo kutoka lebo ya WCB amesema Watanzania wanamchango mkubwa katika mafanikio yake hivyo kuwaomba kuendelea kufuatilia kazi zake.
“Tuzo ya AFRIMMA niliyopata imenipa ari ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili nifike mbali zaidi na hii inaonyesha ni kwa jinsi gani muziki wangu unatazamwa ulimwenguni,” amesema.
Pia amewaasa watoto wa kike wanaochipukia kimuziki wasikate tamaa bali waendelee kupambana ili siku moja waone matunda ya kazi zao.