Watanzania wasisitizwa kuthamini utamaduni

0
497

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe ameendelea kusisitiza kuwa lugha ni kielelezo na sehemu muhimu ya utambulisho wa Taifa lolote duniani.

Dkt Mwakyembe ametoa kauli hiyo jijini Dodoma katika hafla ya kuwatunuku vyeti vya utambuzi wataalamu 67 wa lugha ya kiswahili waliofuzu mafunzo ya muda mfupi yaliyoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).

“Taifa lolote lisilo na utamaduni wake ni taifa mfu, na sisi tunajivunia kwa kuwa na utamaduni hai ikiwemo lugha yetu ya Kiswahili”, amesema Dkt Mwakyembe.

Ameongeza kuwa lugha ya Kiswahili ni kitambulisho cha utamaduni wa Mtanzania , kwa kuwa ndiyo lugha inayowaunganisha watu katika shughuli mbalimbali za Kijamii, Kisiasa na kiuchumi.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa Consolata Mushi amesema kuwa mpaka sasa Baraza hilo limefanikiwa kutoa mafunzo kwa wataalamu 350 wa lugha ya Kiswahili ambapo jumla ya wataalamu 198 tayari wametunukiwa vyeti na wengine 98 wanatarajiwa kutunukiwa vyeti hivyo mwezi Disemba mwaka huu.

Amesema lengo la BAKITA ni kuwapa fursa wataalamu hao ili waweze kusajiliwa katika mfumo wa kanzi data ambayo tayari imesajili wataalamu 380 kwa ajili ya kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wageni ndani na nje ya nchi.