‘STILL OKY TO DATE’ ni filamu iliyobeba uhalisia wa maisha ya kila siku ya vijana, inaonesha changamoto wanazopitia na namna wanavyopambana kuzimudu changamoto hizo.
Mtayarishaji mkuu wa filamu ya ‘STILL OKY TO DATE’ ni
Kefa Ogilo ambaye
pia ni mtumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Filamu hiyo ambayo Kefa ameitayarisha kwa kushirikiana na Jerryson Onasaa na kuongozwa na Mathew Valerian, imekuwa gumzo kutokana na mvuto wa simulizi yake na ubora wa filamu hiyo.
Pia imeigizwa na Issa Mbura ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Sanaa Bunifu.
Waigizaji wengine ni Tunu Mbegu ambaye ni mshindi wa tuzo ya muigizaji bora wa kike ZIFF 2022.
Pia Collins Franks na Catherine Michael ambao ni wahamasishaji maarufu wa mtandao wa Tiktok.
Kefa ameamua kutumia kipaji chake na ujuzi alioupata darasani kuisuka filamu hiyo ambayo kwa sasa ipo sokoni.
Akizungumza katika mahojiano kwenye kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC 1, Kefa amesema kazi ya uandishi wa makala za filamu ni kitu anachopenda zaidi kukifanya na kwamba kipo ndani ya taaluma aliyosomea.
Amesema bidii yake ilionekana toka akiwa chuoni ambapo alikuwa akiandika na kutayarisha makala fupi za filamu ambazo ndizo zilimuonesha kuwa ana uwezo na kupitia makala hizo.
Kefa Ogilo amesema alikuwa akitumia muda wake wa ziada kuandika makala kila siku na baadae alipata wazo la kuandaa filamu ya ‘STILL OKY TO DATE’ na kuwashirikisha rafiki zake ambao nao walikuwa na hamasa ya kutengeneza filamu.
Katika filamu hiyo yumo mwalimu aliyemfundisha Kefa moja ya masomo ya uandaaji wa filamu.
Kefa amesema haikuwa rahisi kuandika makala na kumpa mwalimu wake aigize ambaye ni mbobezi katika masuala ya filamu, ila kutokana na alivyokuwa ameisuka makala hiyo alijua kwa uhakika mwalimu wake hatochomoka kwenye ombi hilo.
Kwa mujibu wa Kefa, imemchukua takribani miaka miwili kuandaa filamu hiyo ya ‘STILL OKY TO DATE’ hadi kukamilika ambapo kwa sasa inawezwa kutazamwa kupitia chaneli ya Maisha Magic Movies.