Idris Sultan aachiwa kwa dhamana

0
1043

Msanii wa Vichekesho, Idris Sultan na mwenzake Innocent Maiga wamesomewa mashitaka mawili katika Mahakama ya Kisutu ikiwemo kushindwa kufanya usajili wa simu kadi iliyokuwa inamilikiwa na Mtu mwingine, kosa hili linamkabili Idris, ambapo inadaiwa alitumia kadi ya simu iliyomilikiwa na Innocent Maiga bila kuripoti kwa mtoa leseni.

Mahakama ya Kisutu imesema kosa jingine ni kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya mtumiaji wa kadi ya simu linalomkabili Innocent Maiga.

Baada ya kusomewa mashitaka yao, Idris na mwenzake Maiga, wamekana makosa yao, ambapo upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili, waliosaini bondi ya Tsh. Mil 15 kila mmoja.

Wakili wa Idris, Benedict Ishabakaki ameondolewa kumuwakilisha Idris kwasababu atatumika kama sehemu ya ushahidi wa upande wa Jamhuri kutokana na kushuhudia mshitakiwa wake akichukuliwa maelezo Polisi, hivyo anabakia Wakili Jebrah Kambole.

Kesi imeahirishwa hadi Juni 9, 2020.