Mmoja wa Mameneja wa kundi la Wanamuziki la Wasafi (WCB) Sallam amesema kuwa, Mwanamuziki Rajab Abdul maarufu kama Harmonize, tayari ametuma ombi la kuvunja mkataba wake na kundi hilo.
Akizungumza katika mahojiano maalum katika kipindi cha Block 89 kinachotangazwa na Redio ya Wasafi, Sallam amesema kuwa wana mpango wa kukutana na Harmonize ili kujadili jambo hilo.
Amesema kimaandishi Harmonize yupo WCB, lakini kiuhalisia hayupo kwenye kundi hilo na katika matamshi yake ameeleza kuwa yupo tayari kupitia sheria na uraratibu kuvunja mkataba wake na Lebo hiyo ya WCB .
Taarifa za Harmonize kujiondoa katika Lebo hiyo ya Wasafi zilianza kuenea kufuatia kutoonekana kwenye tamasha la Wasafi kama ilivyotarajiwa na pale alipoamua kubadili wasifu wa ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.
Sallam amekiri kuwa uongozi wa Wasafi hauna pingamizi kufuatia maamuzi ya Harmonize na wamependezwa na kitendo cha msaanii huyo cha kutaka kusimama peke yake.
Kundi la Wasafi linaundwa na wasanii mbalimbali akiwemo Abdul Nasib maarufu kama Diamond Platinums, Rayvanny ,Queendarleen ,Mbosso na Lover lover.