Harmonize aachia filamu ya Single Again

0
850

Mwanamuziki Rajab Kahali almaarufu Harmonize, Konde Boy, Jeshi, anayetamba na wimbo wa ‘Single Again,’ ameachia filamu fupi ya uhalisia wa yaliyomsibu kwenye mapenzi katika chaneli yake ya YouTube.

Katika filamu hiyo inayotokana na wimbo wake wa ‘Single Again’ yenye dakika 5 na sekunde 41 imeangaliwa zaidi ya mara 10,000, anaelezea kuwa ameachana na mpenzi wake na sababu za kuachana.

Anaoneshwa akiwa ufukweni amejawa na mawazo na kuanza kumsimulia Director Kenny kuwa alidhani amepata mke, alikuwa tayari kuanzisha familia na tayari akamtambulisha kwa mama yake.

Ugomvi mkubwa ulianza asubuhi moja baada ya kuzifuma meseji za kimapenzi kati ya mpenzi wake wa pekee na jamaa mwingine.

Wimbo wa Single Again umetoka si muda mrefu baada ya Konde Boy kuvunja uchumba wake na Kajala, uhusiano uliotikisa mitandao ya kijamii. Je! Hadithi hii ya kweli inaweza kuwa inamhusu mwanamama huyo?