Ghetto Kids wang’ara BGT

0
578

Kikundi cha kucheza muziki cha Triplets Ghetto Kids cha nchini Uganda, kimetikisa shindano la ‘Britain’s Got Talent’s’ ( BGT) 2023 kwa kuwashangaza majaji na watu mbalimbali kilipokuwa kikitumbuiza katika shindano hilo.

Ghetto Kids wamepata heshima ya kubonyezewa king’ora cha dhahabu
‘The Golden Buzzer’, baada ya uchezaji wao kuwavutia watu wengi walioshiriki katika shindano hilo huko nchini Uingereza.

King’ora hicho cha dhahabu kilibonyezwa kabla ya muda na Jaji Bruno Tonioli, ambaye ni Jaji mpya kwenye shindano hilo la Britain’s Got Talent’s.

“Ilinibidi tu nibonyeze king’ora. walikuwa na maajabu sana”. Amesema Jaji Bruno

‘Golden buzzer’ inabonyezwa na majaji wa shindano endapo wanataka mtu au kundi kuvushwa hatua kadhaa hadi kufika hatua ya nusu fainali.

Majaji wote wanne katika shindano hilo wanakuwa na ving’ora vyenye rangi nyekundu ambavyo huvitumia kupiga kura na endapo ving’ora vyote vinne vyekundu vitamulika alama.ya X juu ya jukwaa, mshiriki anakuwa hajakidhi vigezo vya kuwa mshindani.

Mshindi wa BGT 2023 atajinyakulia zawadi ya pesa taslimu Pauni 250,000 ambazo ni sawa na shilingi 725,276,169.50 pamoja na nafasi ya kutumbuiza mbele ya mwakilishi kutoka familia ya Kifalme nchini Uingereza siku ya fainali Novemba 30 mwaka huu katika ukumbi wa Royal Albert.