COSOTA yahamia rasmi wizara ya Habari

0
265


 
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe amesema kuwa lengo la kuihamisha Taasisi ya Hakimiliki (COSOTA) kutoka wizara ya Viwanda na Biashara kwenda wizara  anayoisisimamia ni kuhakikisha wadau wa sanaa wanapata huduma sehemu moja  kwa sababu asilimia 86 ya wadau wake ni wasanii.

Dkt Mwakyembe ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari na kuongeza kuwa tayari Rais John Magufuli amesaini waraka unaogawa majukumu kwa wizara kuruhusu mabadiliko hayo muhimu ambayo yanawagusa wabunifu,watunzi, waandishi wa vitabu,kazi za sanaa na sanaa na jadi.

“Namuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hii ndani ya saa ishirini na nne awe amekutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ili waweze kukabidhiana nyaraka muhimu za uendeshaji wa COSOTA”amesema Dkt Mwakyembe.

Amesema uwepo wa COSOTA katika wizara ya Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo utarahisisha ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) katika kulinda na kusimamia maslahi ya wasanii wa filamu na muziki pamoja na kupanua wigo wa malipo na stahili za wasanii kwa kazi zao katika majukwaa mbalimbali ya sanaa kielektroniki.

Waziri Mwakyembe amesisitiza kuwa, lazima COSOTA ya sasa iingie mikataba na nchi za nje ambazo vyombo vyake vya habari vimekua vikipiga muziki wa wasanii wa Tanzania bila kuwapatia gawio au kufaidika kwa namna yoyote ile.