BASATA: Haiwezekani Msanii kuondolewa kwenye tuzo

0
585

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limesema kuwa kwa sasa haiwezekani msanii yeyote kuondolewa kwenye mfumo wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2022, na hivyo limewataka wasanii kujitangaza ili waendelee kupigiwa kura za kutosha.

Taarifa ya BASATA imekuja kufuatia malalamiko ya baadhi ya wasanii na wadau wa sanaa ambapo wamehoji namna walivyoshiriki kwenye vipengele mbalimbali huku wengine wakiomba kuondolewa kwenye orodha.

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa mchakato wa usajili ulifanyika kwa siri ambapo mwanamuziki alisajili na kupakia taarifa zake ikiwemo nyimbo na vipengele anavyotaka kuwania.

“BASATA inawasisitiza wadau wa sanaa kuwa haihusiki na kuingiza taarifa wala kumchagulia msanii kipengele cha kuwania tuzo,” imeeleza taarifa hiyo.

Baadhi ya wasanii waliotoa malalamiko hayo ni mwanamuziki Rayvanny ambaye kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika “TMA we are proud [tuna furahia] kwamba muna support [unga mkono] mziki wetu…. But HIKI SIO NILICHOTEGEMEA. Am not happy [Sijafurahia].”

Kwa upande wake Mbosso ameeleza kushangazwa na ‘EP’ yake kutokuwepo kwenye tuzo hizo, huku akishutumu waandaaji kuendekeza roho mbaya, chuki na kwamba wamewashirikisha wasanii wanaoweza kuwatumia watakavyo.