Avunja rekodi kwa kucheza muziki siku 5

0
784

Mwanafunzi Srushti Sudhir Jagtap (16) raia wa India, amevunja rekodi ya dunia ‘Guinness World Records’ baada ya kucheza muziki kwa muda wa siku tano mfululizo.

Srushti alianza kucheza muziki asubuhi ya Mei 29, 2023 na kuendelea hadi alasiri ya Juni 03, 2023, huku akipewa muda wa dakika tano za kupumzika ndani ya kila saa moja.

Rekodi ya Srushti imerekodiwa kuwa amevunja rekodi kwa kuwa mtu binafsi aliyecheza kwa muda mrefu zaidi ambao ni saa 127.

Ukumbi uliotumika kwa ajili ya kucheza muziki huo ni wa chuo anachosoma Srushti, ambao ulijaa wafuasi wake wengi pamoja na wazazi wake ambao walikuwa wakimtia moyo katika safari yake hiyo ya kutaka kuvunja rekodi ya dunia.

Alicheza kwa mtindo wa kitamaduni wa Kihindi wa Kathak akichanganya na Yoga.

Srushti amevunja rekodi ya awali ya saa 126 iliyowekwa na mchezaji wa muziki wa Nepal, Bandana Nepal mwaka 2018.