ZSSF yaagizwa kusimamia amana za Wanachama

0
187

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi amesema kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ili kuhakikisha amana zote za Wananchama zinasimamiwa ipasavyo.

Dkt Mwinyi ametoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa jengo jipya linalojulikana kama Hifadhi Building, linalomilikiwa na ZSSF lililoko Tibirinzi wilaya ya Chake Chake mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha inachukua hatua zinazofaa na kwa wakati, kuhakikisha ZSSF inaendelea kuimarika, inaongozwa na kusimamiwa na Viongozi walio makini na wanaojiepusha na vitendo vya ubadhirifu, rushwa na wizi.

Dkt Mwinyi pia amewataka Viongozi wa Mfuko huo kuhakikisha kuwa utekelezaji wa dhamira njema ya kutumia amana za Wanachama wa Mfuko wanayokusanya iambatane na mipango imara ya kusimamia uwekezaji huo.

Ufunguzi wa jengo hilo ambao ni sehemu ya sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, umehudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, -Maalim Seif Sharif Hamad.