Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Dustan Kyobya amewataka wawekezaji katika bandari ya Mtwara wakiwemo wa makaa ya mawe kutoa ajira kwa vijana wa Mtwara ili nao wafaidike na uchumi unaozidi kuongezeka kutokana na biashara kwenye bandari hiyo.
Kyobya ametoa wito huo wakati akishuhudia meli mbili zilizofika katika bandari ya Mtwara kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe tani zaidi ya elfu tisini kwenda kwenye nchi za Poland na Uholanzi.
Amesema wawekezaji wote wanaotumia bandari ya Mtwara ni vema wakahakikisha wanatoa ajira kwa vijana.
Kaimu Meneja wa bandari ya Mtwara, Teddy Kololo amesema, meli hizo zimefika bandarini hapo kusafirisha makaa ya mawe zaidi ya tani elfu tisini, ambapo meli moja itasafirisha tani elfu 34 kwenda Poland na tani elfu 57 zitasafirishwa kwenda Uholanzi.
Kololo amesema ujio wa meli hizo mbili unafanya jumla ya meli nne ambazo zimehudumiwa ndani ya mwezi huu wa Septemba katika bandari ya Mtwara na kusafirisha tani laki mbili kwa mwezi huu pekee.