TRA yatakiwa kupiga mnada makontena ya samani

0
533

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango amemuagiza Kamishna wa forodha wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kufuata hatua stahiki na kuyapiga mnada makontena Ishirini ya samani yaliyoagizwa na kuingizwa nchini na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, – Paul Makonda ambayo hayajalipiwa kodi.

Waziri Mpango ametoa agizo hilo bandarini jijini Dar es salaam ambapo amefanya ziara ya kushtukiza na kutoa wito kwa watanzania kununua samani hizo pindi zitakapopigwa mnada kwa mara nyingine.

Ziara hiyo ya Waziri Mpango ilikua na lengo kupata taarifa ya makontena hayo Ishirini ambayo yaliingia katika bandari ya Dar es salaam kwa awamu mbili tofauti tangu mwezi Januari mwaka huu na kutakiwa kulipiwa kodi ya zaidi ya Shilingi Bilioni Moja.

Makontena hayo Ishirini ya samani yanatarajiwa kupigwa mnada na TRA na endapo yatakosa mteja yatatolewa msaada kwa shule na ofisi mbalimbali nchini.