Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kinatarajia kuanza kutumia mfumo wa ndani wa kielektroniki kutoa vibali vya kazi kwa wawekezaji, lengo likiwa ni kuwawezesha wawekezaji hao kuomba vibali hivyo kabla ya kufika nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, – Geoffrey Mwambe amesema kuwa hatua hiyo itawezesha maombi hayo kufanyiwa kazi mapema na kuondoa usumbufu kwa wawekezaji hao pindi wanapofika nchini.
Kwa mujibu wa Mwambe, mfumo huo utaanza kutumika Septemba Tatu mwaka huu.
Mwambe pia amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo baadhi ya wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na mawaziri kuacha kutoa matamko na maagizo kwa wawekezaji nchini.
Amesema kuwa ni vema kila mamlaka ikatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kufafanua kuwa iwapo kuna tatizo lolote linalohusu kodi, vibali au ubora wa bidhaa kwa Mwekezaji kuna haja ya kufuata taratibu kutafuta ufumbuzi kupitia mamlaka husika badala ya kutoa maagizo ambayo hayazingatii sheria.