Microsoft kufikisha intaneti Afrika kupitia Satelaiti

0
316

Kampuni ya kiteknolojia ya Microsoft imeweka bayana mpango wake wa kufikisha huduma ya intaneti kwa njia ya satelaiti kwa watu zaidi ya milioni 10 ambao nusu yake wanaishi katika nchi za Afrika.

Mpango huo wa kampuni ya Microsoft una lengo la kuziba mwanya wa kidijitali na ulimwengu unaoendelea.

Katika mkutano wa viongozi wa bara la Afrika na Marekani unaoendelea Washington D.C, kampuni hiyo imesema itaanza mradi wa satelaiti hivi karibuni huku ikiweka kipaumbele cha kuunganisha intaneti kwa mara ya kwanza kwenye nchi za Misri, Senegal na Angola.

Hata hivyo kampuni hiyo ya kiteknolojia ya Microsoft imeweka wazi mpango wa kupanua shughuli zake nchini Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kutoa muunganisho wa intaneti katika sehemu za mbali zaidi za Marekani, Guatemala na Mexico kwa kushirikiana na mtoa huduma za setilaiti Viasat.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2025, mradi huo utatakiwa uwe umetoa muunganisho wa mtandao kwa robo ya watu takribani bilioni moja duniani kote.