Daraja la mto Rau laanza kukarabatiwa

0
2401

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kilimanjaro umeanza ukarabati wa daraja la Mto Rau lililoko Manispaa ya Moshi kufuatia kingo za daraja hilo kuathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha, ili kunusuru kukatika kwa mawasiliano.

Msimamizi wa Kitengo cha Matengenezo ya Barabara TANROADS mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Bernitho Mtovela amesema, kwa muda wa siku tano watahakikisha ukarabati wa daraja hilo umekamilika.

Amesema kinachofanyika ni kujaza mawe pamoja na kuweka zege katika kingo za daraja hilo ili liwe imara na lisiweze kuleta madhara mengine kwa watumiaji wa barabara hiyo ya mikoa ya kanda ya Kaskazini.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amekagua ukarabati wa
daraja hilo la Mto Rau na kuwahakikishia wananchi kuwa hakuna shughuli yoyote itakayosimama wakati ukarabati huo ukiendelea.