Tanzania imeikaribisha Canada kushiriki katika kuimarisha uchumi wa buluu kwa kutumia uzoefu wa nchi hiyo pamoja na kukaribisha wawekezaji katika sekta hiyo.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Ahmed Hussen Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo Mei 16, 2024.
Makamu wa Rais amesema kwa sasa Tanzania ni sehemu sahihi zaidi kuwekeza kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza katika kuimarisha uchumi pamoja na kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji na biashara kwa kufanya mageuzi ya kitaasisi, kisera na kuimarisha utawala wa demokrasia.
Aidha amesema Serikali ya Canada inaweza kushirikiana zaidi na Tanzania katika sekta ya afya kwa ujenzi wa viwanda vya kuzalisha dawa, kuwekeza katika makao makuu ya nchi Dodoma katika ujenzi wa miundombinu, udhibiti wa taka ngumu, viwanja vya michezo pamoja na mazao ya mbogamboga.
Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina yake na Canada na kuishukuru kwa kuiunga mkono Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, biashara na uwekezaji, kilimo pamoja na ulinzi na usalama.
Dkt. Mpango pia ameishukuru Serikali ya Canada kwa kuunga mkono ajenda ya Rais Samia ya nishati safi ya kupikia. Amesema kuunga mkono jitihada hizo kutaharakisha wananchi wa Tanzania kuondokana na nishati isiyofaa ya kupikia na kufikia malengo ya mkakati wa kitaifa wa kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Kwa upande wake, Waziri huyo wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Ahmed Hussen amesema uhusiano wa Tanzania na Canada ni wa muda mrefu katika hali zote ambao umeendelea kuimarika. Amesema katika wakati huu ambao Tanzania imefikia uchumi wa kati wa chini ni muda mwafaka wa kuongeza ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.
Amesema katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi Canada inatambua umuhimu wa kufanya kazi pamoja ili kuondoa athari zinazotokana na mabadiliko hayo kwa wananchi.