Tanzania na Rwanda zatatua changamoto katika mpaka wa Rusumo

0
1092

Wajumbe kutoka Tanzania na Rwanda wamekubaliana kuwasiliana kabla ya kuweka mwongozo mpya wa afya na mizigo unaoweza kuathiri mizigo inayovuka mpaka katika kukabiliana na COVID-19.

Azimio hilo na mengine yamefikiwa katika kikao cha pamoja kati ya nchi hizo mbili ambacho kimefanyika Mei 15 mwaka huu kwa njia ya video ili kujadili namna ya kuondoa shehena zilizokwama katika Mpaka wa Rusumo.

Mbali na hilo, maafisa wa Tanzania na Rwanda wamekubaliana kuwa madereva wataruhusiwa kulala nchini Rwanda katika maeneo yaliyotengwa kwa gharama zao, magari ya bidhaa zinazoharibika na bidhaa za petroli yataruhusiwa kuingia kuanzia saa 12 alfajiri hadi saa 12 jioni huku yakisindikizwa bure.

Aidha, wajumbe hao wamekubaliana kuwa katika kuzuia kusambaa kwa Corona mipakani, madereva wa magari makubwa watapimwa kabla ya kuanza safari nchini Tanzania, na Rwanda watatoa vipimo kwa madereva watakaokuwa wakiendelea na safari kwenda nchi nyingine na wale wa bidhaa zinazoharibika.