Tanzania kupokea Watalii 10,000 kutoka Shanghai

0
1626

Bodi ya Utalii Nchini (TTB) imesaini makubaliano na kampuni ya Touchroad International Group ya nchini China kwa ajili ya kusafirisha watalii elfu kumi kutoka jiji la Shanghai kutembelea Tanzania mwaka 2019 kwa kutumia ndege maalum.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kuwa makubaliano hayo yamesainiwa wakati wa mikutano ya kutangaza utalii wa Tanzania katika soko la China.

Mikutano hiyo ni matokeo ya jitihada za balozi wa Tanzania nchini China kwa kushirikiana na TTB ambapo katika mkutano wa kwanza uliofunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Aloyce Nzuki, zaidi ya washiriki mia mbili wamejitokeza zikiwemo kampuni za utalii, mawakala wa usafirishaji, mashirika ya ndege na vyombo vya habari.

Wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii nchini Devotha Mdachi ametoa mada maalum kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo nchini pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii, huku kampuni za utalii kutoka Tanzania zikipata fursa ya kuelezea gharama zao za utalii kwa soko la China.

Nalo Shirika la Ndege nchini (ATCL) limetumia mkutano huo kutangaza mpango wake wa kuanza safari za moja kwa moja kutoka Tanzania hadi China katika mji wa Guangzhou mwezi Februari mwaka 2019.

Mikutano ya kutangaza utalii wa Tanzania katika soko la China inaendelea katika miji mingine nchini humo ikiwa ni pamoja na Guangzhou, Hong Kong, Chengdu na Beijing.