Tanzania kuingiza bidhaa Marekani bila ushuru

0
879

Tanzania mwaka huu imekuwa miongoni mwa nchi za Afrika zinazostahili kupeleka bidhaa zake za kilimo nchini Marekani bila kutozwa ushuru kupitia Mpango wa kuinua biashara na Afrika wa AGOA (Africa Growth and Opportunity Act).

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula baada ya kukutana kwa mazungumzo na Balozi wa Marekani hapa nchini, Dkt. Donald J. Wright, jijini Dodoma.

“Hii ni fursa muhimu kwetu na kinachotakiwa sasa ni sisi kujiimarisha katika kuzalisha bidhaa bora zitakazokidhi vigezo vya kuingia kwenye soko la Marekani,” amesisitiza Waziri Mulamula.

Katika mkutano huo wawili hao wamezungumzia pia masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo mpango unaofadhiliwa na Marekani wa kupambana na UKIMWI wa PEPFAR.

Balozi Wright ameeleza kuwa Marekani ipo tayari kushirikiana na Tanzania na kwamba kampuni nyingi za nchi hiyo zipo tayari kuja kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini wakati wowote kuanzia sasa.

Marekani inaihesabu Tanzania kama rafiki na mshirika muhimu hivyo mkutano huu ni moja ya jitihada za kuimarisha ushirikiano na urafiki huo,” ameeleza Balozi Wright.