Tanzania kinara kwa kuvutia wawekezaji

0
1735

 

Tanzania imeendela kuweka rekodi ya  kuvutia wawekezaji kwa nchi zilizopo ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa na mtaji wa uwekezaji wa Dola Bilioni 1.18 za Kimarekani ikifuatiwa na Uganda wenye uwekezaji wa Dola Milioni 700 za Kimarekani.

Akizungumza na waandishi wa habari  Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu  wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) Godffrey Mwambe amesema kuwa Kenya inashika nafasi ya Tatu ikiwa na uwekezaji wa Dola Milioni 670 za Kimarekani.

Mwambe amesema kuwa Tanzania inaongoza kwa kuvutia wawekezaji kutokana  na mapinduzi makubwa yaliyofanywa na serikali ambapo hadi sasa imewekeza jumla ya miradi mipya 905 katika sekta mbalimbali, miradi ambayo itatengeneza ajira 115,055 kwa watanzania na kuleta tija na manufaa kwa Taifa.

Ametolea mfano miradi mikubwa iliyowekezwa nchini kuwa ni pamoja na kiwanda cha Goodwill Ceremics Ltd kilichopo Mkuranga mkoani Pwani kinachojihusisha na utegenezaji vigae ambacho kimewekeza jumla ya Dola milioni 53 za Kimarekani na kutoa ajira za moja kwa moja 1500 kwa Watanzania na ajira zisizo za moja kwa moja 3,000.

“Viwanda vingine ambavyo vimeiwezesha Tanzania kuwa kinara wa kuvutia wawekezaji ni KEDA (Twyford) Tanzania ceramic Ltd pia ni cha kutengeneza marumaru na hiki ni kikubwa zaidi kina mtaji wa Dola za kimarekani milioni 56, kimetoa ajira  za moja kwa moja zipatazo 2,000 kwa watanzania na  ajira zisizo za moja kwa moja 4,000” amesema Mwambe.

Mkurugenzi Mkuu  huyo wa Kituo cha Uwekezaji Nchini ametaja nchi zinazoongoza kwa kuwekeza Tanzania kuwa ni pamoja na China, Uingereza  na Marekani.