Taasisi na mashirika yatakiwa kuvutia wawekezaji

0
2360

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) Geoffrey Mwambe ametoa wito kwa taasisi na mashirika ya umma kutathmini mifumo yao ya utendaji kazi na kuangalia maeneo muhimu ya kuyafanyia kazi ili kuharakisha juhudi za kuvutia wawekezaji.

Mwambe ametoa wito huo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ambapo alikua akizungumzia kongamano la uwekezaji lililofanyika mwezi Oktoba mwaka huu huko Geneva, – Uswisi na kuhudhuriwa na wakuu wa nchi na viongozi wakuu wa taasisi za uwekezaji, kongamano lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Biashara(UNCTAD).

Amesema kuwa kila taasisi na shirika la umma nchini lina maeneo muhimu kwa ajili ya kuvutia wawekezaji, hivyo juhudi za dhati zinahitajika katika kuimarisha maeneo hayo ambayo yataimarisha uchumi wa Taifa.

“Kila wizara, kila idara na kila taasisi ya serikali itambue inahitaji kufanya nini ili kuweza kuvutia uwekezaji, kila sekta ijitathmini inafanya nini katika kurekebisha mfumo wao ili  kuvutia wawekezaji, watu wengi wanadhani suala la uwekezaji ni la wizara ya viwanda na Biashara tu,wengine wanadhani ni suala la Kituo cha uwekezaji tu,hapana ni la kila wizara na la kila mtu,  hivyo ni lazima sekta zote zifanye juhudi za kuvutia uwekezaji”, amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TIC.

Amesisitiza kuwa TIC inafanya jitihada nyingi za kuhamasisha wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza nchini, lakini kumekua na baadhi ya watendaji wa serikali wamekua wakikwamisha juhudi hizo, jambo ambalo halikubaliki.

“Jamani huko Duniani tunanyang’anyana wawekezaji, hata nchi zilizoendelea zinahamasisha wawekezaji waende kuwekeza kwao,sisi hapa kwetu tunahamasisha waje na wakija kuna baadhi ya watendaji wa serikali wanawakwaza, hili halikubaliki”, amefafanua Mwambe.

Ameongeza kuwa wakati wa kongamano hilo,  UNCTAD imetoa mwenendo wa uwekezaji kwa nchi  mbalimbali duniani, ambapo kwa mwaka 2016 kwenye nchi za Afrika Mashariki, Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji  kwa kupata  uwekezaji wa shilingi  bilioni 1.565  ikifuatiwa na Uganda kwa shilingi milioni 580.