Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli leo ameweka jiwe la msingi katika Soko Kuu la Kisutu ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu jijini Dar es Salaam.
Soko Kuu la Kisutu lenye ghorofa 4 kwenda juu na 1 kwenda chini (basement) limejengwa upya likiwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 1,500 ikilinganishwa na soko la zamani lililokuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 669, kuegesha magari 40, lina maeneo ya huduma za kijamii na lina eneo la ukubwa wa meta za mraba 11,935.
Akihutubiwa wananchi amesema kuwa takribani 70% ya Watanzania ni wakulima na uwepo wa soko kama hili utasaidia wao kupata riziki na kuinua uchumi wa maeneo yanayonufaika na mradi huu.
“Masoko ni kiungo muhimu sana katika mnyororo wa uzalishaji na biashara,” amesema Rais Magufuli.
Ujenzi wa soko hilo ni sehemu ya masoko 22 yanayojengwa nchini kote ambapo mbali na hayo, stendi za magari 18 zimejengwa hatua inayolenga kuboresha miji yetu.
Rais Magufuli ameendelea kusisitiza usawa katika miradi hii inayoendelea kutekelezwa na Serikali na kusema kuwa ni matumaini yake kuwa soko halitobagua baadhi ya Watanzania.
Soko la Kisutu ni miongoni mwa miradi saba ya kimkakati inayotekelezwa na serikali mkoani Dar es Salaam ikiwepo mradi wa soko Kigamboni, Mburahati, machinjio ya Vingunguti na soko katika stendi mpya ya Magufuli, Mbezi.
Kwa upande mwingine Rais Magufuli amewataka viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge na madiwani kwenda kwenye maeneo yao kusikiliza kero za wananchi na wananchi kwenda kwenye ofisi za viongozi wa maeneo yao wawapo na shida pasi na kumsubiri yeye.
Rais amemtaka mkandarasi wa soko hilo kukamilisha ujenzi ndani ya tarehe alizopewa (Machi 2021).