Serikali yazindua kituo chake cha kwanza cha kuuza mafuta

0
1889

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi biashara ya kuuza na kusambaza mafuta nchini kwa kufungua kituo cha kwanza kuuza mafuta ya petroli na dizeli cha Serikali kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kupitia Kampuni yake Tanzu ya Mafuta ( TANCOIL).

Aidha Dkt. Kalemani alisema kuwa kuzinduliwa na kufunguliwa kwa biashara hiyo ni kutimiza azma na nia njema ya Serikali ya kuboresha shirika lake la TPDC,kuwapatia na kuwasogezea karibu wananchi wake huduma ya kupata mafuta yenye viwango vya ubora unaotakiwa, bei nafuu, na yatakayopatikana kwa wingi muda wote.

Amesema baada ya kuanza rasmi kwa biashara hiyo, TPDC kupitia TANCOIL itashirikiana na Halmashauri zote nchini kuhakikisha inafanikisha azma ya serikali ya kufungua na kuweka vituo vya kuuza na kusambaza mafuta katika kila halmashauri nchini pamoja na miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta.

“Tumeshaanza biashara ya kuwauzia wananchi wetu mafuta, sitegemei kusikia mafuta yanauzwa kwa bei aghali katika vituo vya serikali, TPDC na TANCOIL mnielewe vizuri hapa! hii haipo na haitakuwepo, lengo letu sisi serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wapata bidhaa bora za mafuta kwa kiwango kinachotakiwa, kwa bei nafuu na yatapatikana kwa wingi wakati wote na huduma hii inapatikani jirani na maeneo yao!,”Amesema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani aliwaeleza watanzania kuwa TPDC na TANOIL watashiriki katika biashara ya uagizaji na usambazaji mafuta kama zinavyofanya kampuni zingine za mafuta nchini ili kuongeza ushindani na kutanua wigo wa kampuni za kizalendo kushiriki katika biashara ya mafuta, ambayo kwa sasa inafanywa na makampuni kutoka nje ya nchi tu.

Alisema kuwa serikali kupitia TPDC itajenga vituo 100 kwa kipindi cha miaka 5 ijayo, tayari baadhi ya Halmashauri zimeanza kutenga maeneo yatakayojengwa vituo hivyo: Aidha itahakikisha kuwa nusu ya mafuta yote yanayoingizwa nchini yanasimamiwa TPDC.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini, (TPDC), Dkt. James Mataragio amesema kuwa katika kutekeleza azma hiyo ya serikali, kuanzia mwaka huu wa fedha 2020/2021, TPDC imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya mtaji wa kugharamia shughuli za uagizaji, usambazaji na usimamizi wa mauzo ya mafuta nchini kote

“Ninafuraha sana TPDC inaandika historia mpya na kubwa sana katika nchi yetu, tunaungana na wakazi wa Mkoa wa Mara, kwa niaba ya Watanzania wote kuonesha furaha yetu katika kuandika historia hii mpya ya kwamba TPDC inarudi kwa kishindo katika biashara ya kuuza na kusambaza wa mafuta ya petroli, dizeli na bidhaa zake kwa maslahi yetu sote na taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Mataragio.

Ameoongeza kuwa Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 imeipa TPDC hadhi ya kuwa Shirika la Mafuta la Taifa (NOC) ili kujiendesha kibiashara, kupitia sheria hiyo, TPDC imeimarisha kampuni zake tanzu za GASCO na TANOIL. Awali, TANOIL ilikuwa COPEC. Kampuni ya GASCO inajishughulisha na biashara ya gesi na TANOIL inajishughulisha na biashara ya mafuta, ambayo ndiyo biashara tunayoizindua leo Kitaifa.

Katika mwaka huu wa fedha, TPDC itakamilisha ujenzi wa vituo viwili katika Mkoa wa Singida na Mkoa wa Geita. Aidha, TPDC inaendelea na mkakati wa kutwaa ardhi katika mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Dodoma na Morogoro. Hatua za utwaaji ardhi katika mikoa ya Dodoma na Tanga zipo katika hatua za ukamilishaji.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, amewaasa wakazi wa wafanyabiashara na watumiaji wa mafuta kuunga mkono juhudi za serikali za kuanzisha bishara ya mafuta kwa kununua mafuta katika vituo vya serikali.