Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya Korosho Nchini ihakikishe inatafuta masoko ya uhakika ya zao hilo, na ambayo yatakuwa na bei nzuri ya kuwanufaisha Wakulima.
Pia, ameitaka bodi hiyo isimamie mwenendo wa ujenzi wa viwanda vidogo na vikubwa vya kubangua korosho katika maeneo yote yanayolima zao hilo, ili kuondokana na uuzwaji wa korosho ghafi.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mkoani Lindi wakati akizungumza na Wakuu wa mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara na Ruvuma, Mrajisi wa Ushirika, Viongozi wa vyama Vikuu vya Ushirika wa Korosho katika kikao kilichohusu upatikanaji wa pembejeo za korosho.
Amesema lazima Bodi ya Korosho nchini ambayo ameizindua iwajibike ipasavyo katika kuhakikisha inaongeza uzalishaji wa zao hilo, na iwapo itashindwa Serikali haitosita kuivunja.
“Lazima mfuatilie na kuufahamu mwenendo wa zao mnalolisimamia, na mjue mfumo unaotumika katika mauzo yake. Pia muwe na takwimu za wakulima na ukubwa wa mashamba yao ili kuweza kuwahudumia kwa urahisi.” Ameagiza Waziri Mkuu