Serikali yaja na mkakati wa kuwainua wakulima wa zao la mkonge

0
981

Serikali kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), kwa kushirikiana na halmashauri mbalimbali nchini ambako zao la mkonge linalimwa imesema itaanzisha vitalu vya zao hilo ili kuwawezesha wananchi kupata mbegu baada ya kuwepo na mwamko wa wananchi kutaka kulima zao hilo.

Akizungumza katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA), Afisa Maendeleo ya Masoko wa TSB, David Maghali amesema kuwa mwamko wa wakulima kulima zao hilo sasa ni mkubwa ndiyo maana Serikali imefikia uamuzi wa kuzalisha miche mingi ili kuwawezesha wananchi kupata fursa katika kilimo cha zao hilo.

“Mwamko wa kuongezeka kwa wakulima wa zao la Mkonge kumekuja baada ya kuongezeka kwa matumizi ya zao hilo hasa kwenye sekta ya ujenzi, kwani mkonge hutumika kutengeneza gypsum na vifaa vya magari kwa hiyo mahitaji yake yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku,” amesema Maghali.

Ameongeza kuwa Maonesho ya Sabasaba yameleta mwamko mkubwa wa wananchi wengi kujua na kujifunza fursa zilizoko kwenye zao la mkonge, ikiwemo kupata elimu juu ya kulima zao hilo, uvunaji wa zao hilo, ajira zinazoweza kutengenezwa katika zao hilo na matumizi yake.

Kwa upande wake Afisa Mipango wa TSB, Fredrick Sospeter amesema,“Ulimaji mkonge ni mzuri kwa sababu zao hili linakomaa kwa muda wa miaka mitatu na baada ya hapo mavuno yake yanachukua hadi muda wa miaka 12 kwa mkulima akiwa anavuna mara mbili kwa mwaka, maana yake akiwa anavuna baada ya miezi sita.”

Zao hilo lina faida nyingi sana ikiwemo mizizi yake ambayo hutumika kutengeneza dawa ya binadamu, mifugo na mimea, shina ambalo hutumika kutenegeneza juisi yenye sukari (asali) ambayo hutumiwa kwa wingi na wagonjwa wenye matatizo ya kisukari, majani yake hutumika kutengenezea nyuzi, kamba, mazulia, magunia, gypsum, karatasi za kutengenezea fedha (noti), gesi, mbolea pamoja na chakula cha wanyama.