Serikali kuendelea kuwalinda Wawekezaji

0
233

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, Serikali itahakikisha inawalinda Wawekezaji  na kulinda bidhaa zao ili waweze kupata soko nchini na nje ya nchi.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti  wilayani Kibaha mkoani Pwani alipotembelea kiwanda cha kuunganisha mabasi cha BM Motors kinachomilikiwa na Mtanzania Jonas Nyagawa na kiwanda cha dawa cha Kairuki, ambapo ameeleza kuridhishwa na uwekezaji katika viwanda hivyo.
 
Amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa lengo la kuinufaisha nchi pamoja na Mwekezaji, hivyo inawakaribisha Wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali.
 
 “Serikali tupo na nyie, maamuzi tuliyofanya ya kuweka mazingira wezeshi ni maamuzi sahihi, tutapita kusikia changamoto za kila mmoja wenu na tutazitatua, ongezeni mitaji kwenye uwekezaji wenu, tumieni taasisi za fedha kuongeza mitaji,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
 
Pia ameziagiza taasisi zote za Serikali zinazohusika na masuala ya uwekezaji zihakikishe Wawekezaji wote walioonesha nia ya kuwekeza nchini wanasaidiwa na kufanikisha mchakato huo bila ya usumbufu wa aina yoyote.

 “Taasisi zote zinazohusiana na uwekezaji zihakikishe kila ambako panatamaniwa na Muwekezaji huduma muhimu zipatikane iwe maji, umeme, barabara na hata viwanja vipatikane kwa urahisi,” ameagiza Waziri Mkuu.

Baada ya kutembelea kiwanda hicho cha kuunganisha mabasi cha BM Motors, Waziri Mkuu Majaliwa alitembelea kiwanda cha dawa cha Kairuki kilichopo katika eneo la Zegereni ambacho kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi Juni mwaka huu.

Akiwa kiwandani hapo, Waziri Mkuu amewahamasisha Wawekezaji kujenga viwanda vya kuzalisha dawa kwa kuwa soko lipo katika hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Gharama ya uwekezaji wa kiwanda hicho ni shilingi bilioni 45 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha chupa za dripu milioni 55 kwa mwaka, ambapo asilimia 60 ni kwa ajili ya soko la ndani na asilimia 40 ni soko la nje.