Serikali kuanza utekelezaji wa mradi wa magadi soda

0
2379

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo amaeeleza kuwa Serikali ipo mbioni kuanza utekelezaji wa mradi wa magadi soda katika Bonde la Engaruka wilaya ya Monduli mkoani Arusha ambao ni moja kati ya miradi 17 ya kimkakati katika kujenga uchumi wa viwanda nchini kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDPIII) 2021/2022 – 2025/2026.

Prof. Mkumbo ameeleza wakati alipotembelea eneo ambalo mradi huo utatekelezwa ambao utekelezaji wake utawezesha ukuaji wa viwanda na uzalishaji wa fursa za ajira.

Mradi huo unasimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo na sasa hatua ya upembuzi yakinifu imekamilika na imeonesha uwepo wa takribani mita za ujazo 3,294,704,894 za magadi hivyo uzalishaji huu utaweza kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi, ukanda wa Afrika Mashariki na soko la kimataifa na utatoa ajira kwa watu wasiopungua 500.

Aidha, Prof. Mkumbo amaeeleza kuwa hatua iliyopo kwa sasa ni kutafuta mwekezaji atakayeshirikiana na Serikali kutekeleza mradi huo na magadi yatakapopatikana yatakuwa malighafi katika mambo mengi kama kutengenezea vioo vya aina zote, Kutengenezea sabuni, karatasi, kusafisha maji, kusafishia madini, kupunguza athari za gesi yenye sumu zinazotoka viwandani na sehemu nyingine nyingi.

Prof. Mkumbo amewatoa hofu wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya mradi kuwa kabla ya mradi huo kutekelezwa mwananchi watapewa elimu kuhusu huo mradi na kila mmoja atalipwa fidia kulingana na tathimini iliyofanyika kwa wananchi wote 599 na ndio mradi utaanza kutekelezwa.