SADC washauri biashara ziendelea kama awali

0
1236

Makatibu Wakuu wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamependekeza kuruhusu biashara za bidhaa zote kuendelea kusafirishwa katika nchi zao kama ilivyokuwa kabla ya janga la virusi vya corona.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam mara baada ya kufungua mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC kwa ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika kwa njia ya video, Katibu Mkuu wa wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Wilbert Ibuge amesema mkutano huo umejadili na kutoa mapendekezo ya kuondoa vikwazo vyote vya kibiashara ili kuweza kuendeleza uchumi ndani ya nchi za SADC.

Balozi Ibuge amesema uamuzi huo utawawezesha wananchi kuendelea na maisha yao ya kawaida na biashara zao kwa kuwa janga la corona litaendelea kuwepo kwa muda ambao ukomo wake haujulikani japo juhudi za kulikabili zinaendelea.

Aidha Balozi Ibuge amesema kuwa ni muhimu kwa nchi wanachama wa SADC kushirikiana na kuhakikisha uchumi wa nchi hizo unakua pamoja na kuwepo kwa janga la virusi vya corona.

Makatibu wakuu wa nchi za SADC walioshiriki mkutano huo ni kutoka nchi za Tanzania ambayo ni Mwenyekiti, Angola, Afrika Kusini, Comoro, Eswatini, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia na Zimbabwe.