Serikali imesema ranchi ya Mkata iliyopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro itakuwa sehemu ya kuzalisha mbuzi kwa wingi, kwa ajili ya mkakati wa kopa mbuzi lipa mbuzi ambao unatarajia kuanza hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika ranchi hiyo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdalllah Ulega amesema ni muhimu kuangalia namna bora ya kufanya ufugaji wa kibiashara katika ranchi ya Mkata.
Amesema Serikali imechagua ranchi hiyo kuwa kituo cha kuzalisha mbuzi kwa wingi, ambao watakuwa wanasambazwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ulega ametembelea kiwanda cha kuzalisha chanjo cha Nobel Vaccine Bioscience (NOVABI) kilichopo mkoani Morogoro, kinachozalisha chanjo za aina ya tatu ikiwemo ile inayotumika kwa ajili ya mdondo, ndui ya kuku na mafua ambayo yanaathiri mfumo wa upumuaji na yamekuwa chanzo kikubwa cha vifo vya kuku.
Akiwa kiwandani hapo Naibu Waziri Ulega ameelekeza chanjo hiyo ya kipekee isambazwe maeneo mbalimbali nchini hasa yale ya vijijini ambayo yana wafugaji wengi wa kuku wa kienyeji.