Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Profesa Elisante Ole Gabriel, ameitaka Benki ya NMB kushirikiana na wizara hiyo katika kukuza sekta ya maziwa nchini kwa kuwa bado kuna mwitikio mdogo wa wananchi kunywa maziwa.
Profesa Ole Gabriel ametoa wito huo jijini Dodoma wakati wa kikao na maafisa kutoka idara ya kilimo ya Benki ya NMB waliofika ofisini kwake kwa lengo la kumwelezea mikakati ya benki hiyo ambayo imekuwa ikifanya tafiti ili kuwekeza katika sekta hiyo ya maziwa.
“Kwa takwimu ambazo zimetolewa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ni kwamba, kwa wastani angalau mtu MMOJA anatakiwa walau atumie lita Mia Mbili za maziwa kwa mwaka, lakini kwa bahati mbaya kwa Watanzania wastani ni lita 47 tu, bado tuna kazi kubwa sana,” amesema Profesa Ole Gabriel.
Amesema kuwa Benki ya NMB inapaswa kuwa na ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia dawati la sekta binafsi, ambalo limekuwa likiwaunganisha wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi ili kuhakikisha mazao yatokanayo na ng’ombe yakiwemo maziwa yanatumika ipasavyo.
Katika kikao hicho ambacho kimehudhuriwa pia na watendaji wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Ole Gabriel ameongeza kuwa wakati umefika kwa Benki ya NMB kushirikiana na wizara hiyo katika kuhakikisha inawaletea maendeleo wafugaji, hasa wadogo ambao wamefanikiwa pamoja na wafugaji ambao watakuwa tayari kubadilika na kuingia katika ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhamahama.
Kwa upande wake Meneja Mwandamizi wa Benki ya NMB kutoka idara ya kilimo, – Carol Nyagaro amesema kuwa kutokana na kasi ya utendaji kazi wa serikali, imeilazimu benki hiyo kubadili mtazamo wa namna ya kutafuta wateja wapya kupitia sekta mbalimbali.
“Kutokana na kasi ya Mheshimiwa Rais John Magufuli na uongozi mzima wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwetu inajenga mazingira mazuri ya kufanya biashara, pia kuchangia maendeleo ya jamii na kuweza kutengeneza wateja wa siku zijazo,” amesema Ngayaro.
Amesisitiza kuwa Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo, inafikiria pia kuwekeza katika sekta ya samaki ambayo imekuwa ikifanya vizuri kiuchumi katika siku za hivi karibuni.