NEEC yatakiwa kuwasaidia vijana

0
2566

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Anthony Mavunde amelitaka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kuhakikisha linawasaidia vijana nchini kushiriki katika uchumi wa viwanda kwa kuwaunganisha na mifuko ya uwezeshaji ili kupata mitaji.

Naibu Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo wakati akifungua maonesho ya ubunifu ya Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri huyo wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira ameonesha kufurahishwa na ubunifu wa wanachuo hao hasa katika mifumo mbalimbali waliyotengeneza ambayo inasaidia kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi katika jamii.

Ametumia maonesho hayo kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi katika shindano la wazo la Biashara lijulikanalo kama Kijana Jiajiri lililo chini ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambapo vijana Kumi washindi kati ya Hamsini watakaochaguliwa watapatiwa mitaji ya kuanzisha Biashara.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi,Makamu Mkuu wa chuo hicho kikuu cha Mtakatifu Joseph Profesa Burton Mwamila amesema kuwa ni dhamira ya chuo hicho kuwa na atamizi (incubation) ya kuwalea na kuwaendeleza vijana hao ili waweze kufikia malengo yao ya kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda.