NBC yakabidhi gawio la Bil 6

0
616

Benki ya NBC imekabidhi Gawio Serikalini la shilingi Bilioni sita, ikiwa ni sehemu ya faida ya shilingi Bilioni 81.9 iliyopatikana kwa mwaka 2022.

Mfano wa hundi ya Gawio hilo imekabidhiwa mkoani Dar es Salaam kwa Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu na Mwenyekiti wa Bodi ya benki ya NBC, Elirehema Dorie.

Akikabidhi mfano wa hundi hiyo Dorie amesema, gawio hilo la shilingi Bilioni sita ni sawa na ongezeko la asilimia 33 ikilinganishwa na gawio la shilingi Bilioni 4 .5 lililotolewa na benki hiyo Serikalini mwaka 2022.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu ametumia hafla hiyo ya kupokea gawio kutoka NBC kuzitaka taasisi zote ambazo Serikali ina umiliki kuhakikisha zinafanya mabadiliko ya kiutendaji kwa kuongeza ufanisi, ili kuiwezesha Serikali kunufaika na uwekezaji huo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC Theobald Sabi amesema, wanahisa wa benki hiyo waliidhinisha gawio la asilimia 30 sawa na shilingi Bilioni 20 ambapo Serikali ikiwa ina umiliki wa asilimia 30 imewaza kupata kiwango hicho cha shilingi Bilioni sita.

Serikali ina umiliki wa hisa za benki hiyo kwa asilimia 30, huku asilimia 55 ikimilikiwa na Absa Group na IFC ikiwa na umiliki wa asilimia 15.