Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeongeza makusanyo ya mapato ya serikali kwenye maeneo ya mipakani mwa Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Mhandisi Nditiye ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye kituo cha huduma cha pamoja cha Mtukula ambacho kinawezesha usafirishaji wa taarifa, data za wateja na bidhaa kutoka Tanzania kwenda nchi jirani ya Uganda.
“Maeneo ya mipakani ndio lango la kuongeza mapato na kukuza uchumi wa nchi yetu, niwatake muendelee na kasi hii ya ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa kutumia Kituo cha pamoja cha huduma ambapo tayari kwa kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka wa fedha wa 2018/2019, mwezi Julai hadi Septemba mwaka 2018 mapato yameongezeka zaidi ya asilimia 100 kwa mwezi na kufikia asilimia 150”, amesema Mhandisi Nditiye.
Kwa upande wake afisa mfawidhi wa forodha wa kituo hicho cha huduma cha pamoja cha Mtukula,- Mohammed Shamte amesema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, malengo yao ni kukusanya shilingi bilioni 15.9 kwa mwaka ambapo tayari imeonekana kiwango hicho kitafikiwa kwa kuwa tayari kwa mwezi wanakusanya shilingi bilioni 1.3.
“Baada ya Serikali kuweka Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, umeongeza spidi na uhakika wa kusafirisha taarifa na data tofauti na hapo awali tulipokuwa tunatumia satelaiti, hivyo mkongo umewezesha ongezeko la mapato”, amesema Shamte.
Naibu Waziri huyo wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amefanya ziara hiyo ya kukagua miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye vituo vya mpakani vya Kabanga, Rusumo Mtukula na Biharamulo.