Marekani Yapongeza Juhudi za Tanzania katika kuvutia wawekezaji

0
2436

Kaimu Balozi wa Marekani nchini Inmi Patterson amesema kuwa nchi hiyo inatambua jitihada za serikali ya Tanzania za kuvutia wawekezaji na kwamba Mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo yatasaidia kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.

Balozi Patterson ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), – Geoffrey Mwambe alipomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kuzungumzia masuala mbalimbali ya uwekezaji ikiwemo  namna bora ya kuvutia wawekezaji wa nje.

Amesema kuwa kufuatia juhudi hizo serikali ya Tanzania za kuvutia wawekezaji, Marekani inaungana na Tanzania katika kuwezesha wawekezaji wengi zaidi kutoka nchini Marekani kuja kuwekeza hapa nchini.

Kaimu Balozi huyo wa Marekani nchini ameihakikishia Tanzania kuwa nchi hiyo itatoa kila aina  ya ushirikiano ili kufanikisha Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda.

“Ubalozi wa Marekani, nchi ya Marekani na Wamarekani wote waliopo nchini Tanzania wapo tayari kusaidiana na serikali katika kuhakikisha nchi ya viwanda inafanikiwa,” amesema Kaimu Balozi Patterson.

Ameishauri serikali ya Tanzania kuwa ili ifanikiwe kwenye uchumi wa viwanda ni vema ikaendelea kushirikiana ba sekta binafsi katika kufanikisha uwekezaji na kueleza furaha yake kutokana na mazungumzo ambayo ya serikali ya Tanzania imekua ikiyafanya kati yake na sekta binafsi.

“Hakuna nchi ambayo inaweza kufikia uchumi wa viwanda bila kushirikisha sekta binafsi  pamoja na wawekezaji wa ndani na nje, hivyo ni vema sekta binafsi ikapewa fursa katika uwekezaji ili kufikia nchi ya Viwanda ambayo sisi tunaiunga mkono kwa nguvu zote,” ameongeza Dkt Patterson.

Kuhusu mazungumzo yao amesema yamejikita katika kukuza biashara, uwekezaji na kukuza uchumi na kwamba kutokana na mazingira mazuri yaliyopo ni imani ya Marekani kuwa Tanzania itafikia kuwa nchi ya viwanda.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini  Geoffrey Mwambe amesema kuwa jukumu la kituo hicho ni kukutanisha sekta mbalimbali za serikali na binafsi ambapo mabalozi wa Tanzania waliopo katika nchi mbalimbali wanahakikisha wanashiriki kikamilifu kuvutia wawekezaji.

Amesema  kuwa jitihada za Kaimu Balozi huyo wa Marekani nchini zimesaidia kufanikisha ujio wa kundi la wafanyabiashara wa Florida kuja nchini kwa ajili ya kuangalia mazingira ya uwekezaji na kwamba wanatarajia kuja nchini hivi karibuni.