Kampuni ya wazawa ya Jitegemee Holdings Company Ltd inayojihusha na uchimbaji wa madini imeanza kusafirisha makaa ya mawe tani elfu 22 kupitia bandari ya Mtwara kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Makaa hayo ya mawe yameanza kusafirishwa ukiwa umepita mwaka mmoja baada ya kampuni hiyo kuanza shughuli za uchimbaji na uuzaaji wa makaa hayo katika viwanda vya Tanzania, Kenya na Uganda.
Akizungumzia hatua hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jitegemee Holdings Company Ltd Emmanuela Kaganda amesema, kampuni hiyo imeingia katika historia ya kusafirisha makaa nje ya nchi baada ya kuwa inauza katika viwanda vya hapa nchini pamoja na nchi jirani za Kenya na Uganda ambapo ilikuwa ikisafirisha kwa njia ya barabara.
‘’Safari hii tumepata bahati ya kuweza kusafirisha makaa ya mawe kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), mwezi ujao tutaondoa meli nyingine ya tani 40,000 kuelekea Falme za Kiarabu kwenye kiwanda cha Saruji, mwezi huo huo pia (Oktoba mwaka huu) kuna mteja mwingine ambaye atasafirisha tani 50,000 kuelekea Ulaya.’’ amesema Kaganda
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas ameipongeza kampuni hiyo ya Jitegemee kwa kuona fursa ya kutumia bandari ya Mtwara kusafirsha makaa hayo kwani amefarijika kuona kuwa ni kampuni ya kwanza ya Kizawa iliyothubutu kufanya uwekezaji huo mkubwa wa biashara ya makaa ambayo yana soko kubwa duniani na anapata faraja kuona bandari inaanza kufunguka.
Ametoa rai kwa wasafirishaji wengine wa bidhaa nyingine ambazo nyingi zinapatikana katika mkoa wa Mtwara zikiwemo korosho, kuendelea kutumia bandari ya Mtwara kwa sababu kuna uwekezaji mkubwa uliofanyika uliogharimu shilingi bilioni 157.