Korosho iliyobanguliwa Tanzania kuuzwa Marekani

0
1517

Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha asilimia 60 ya korosho zote zinazozalishwa nchini zinabanguliwa ufikapo msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026.

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde ameyasema hayo mara baada ya kushuhudia tani 7.5 za korosho zilizobanguliwa zikisafirishwa na kampuni ya Ward Holding Tanzania (WHT) kwenda nchini Marekani.

“Tunashuhudia tukio la kihistoria, ambapo korosho iliyobanguliwa nchini Tanzania inaenda kuuzwa kwa mtumiaji wa mwisho nchini Marekani. Hii ni habari njema kwa wakulima wa korosho nchini na ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na serikali.” amesema Naibu Waziri Mavunde

Kwa upande wake Rais wa kampuni ya WHT Godfrey Simbeye amesema, mahitaji ya korosho iliyobanguliwa nchini Marekani ni karibu mara nne ya korosho inayozalishwa nchini kwa sasa.

Bei ya korosho ghafi nchini ni kati ya shilingi 1,800 na shilingi 2,200 kwa kilo, ambapo unahitaji kilo tano za korosho ghafi ili kupata kilo moja ya korosho iliyobanguliwa.

Kwa korosho iliyobanguliwa nchini Marekani, bei yake ni dola 40 kwa kilo ambayo ni sawa na zaidi ya shilingi elfu 90.