Huduma za mawasiliano vijijini kuboreshwa

0
3285

Katibu Mkuu wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali itatenga fedha ili kuboresha huduma za mawasiliano vijijini kikiwemo kijiji cha Msomera pamoja na kukamilisha zozi la anwani za makazi.

Dkt. Yonazi ametoa kauli hiyo mkoani Tanga alipotembelea kijiji cha Msomera wilayani Handeni, mahali panapojengwa makazi ya kudumu ya wananchi watakaohamia kutoka hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Amesema eneo la Msomera ni la kimkakati huku kijiji chake kikiwa ni cha mfano ambacho Serikali imefuata taratibu zote hasa ujenzi wa miundombinu ya shule, huduma za afya, maji, umeme na imejenga makazi ya kudumu kwa kufuata mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Tayari ujenzi wa nyumba 103 umekamilika katika kijiji hicho cha Msomera na nyingine zinaendelea kujengwa ili Wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro waweze kuhamia na kupisha shughuli za uhifadhi.