BRELA yatoa tamko kuhusu Kalynda

0
1364

Wakala wa Biashara na Usajili wa Leseni (BRELA) imetoa ufafanuzi kuhusu kampuni ya Kalynda E-Commerce Limited kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu uhalali wa biashara inayofanywa na kampuni hiyo.

Kampuni ya Kalynda ilisajiliwa kufanya shughuli za uuzaji wa jumla wa vifaa vya kielektoniki na mawasiliano pamoja na ufanyaji wa biashara ya kiteknolojia ya kimataifa ya mtandaoni.

Taarifa ya BRELA imesema kuwa kumekuwa na taarifa zisizo rasmi zinazoleta taharuki kwenye jamii kuwa Kalynda E-Commerce Limited imekuwa ikifanya biashara ya upatu ya kukusanya fedha kutoka kwa wananchi kwa ahadi ya kupata faida ndani ya muda fulani kinyume na bidhaa au huduma iliyoombewa kupata leseni.

BRELA imetoa angalizo kwa wananchi kuwa, kabla ya kuingia kwenye mahusiano ya kibiashara na kampuni yoyote ni vema kupata uthibitisho wa uhalali na uwepo wa kampuni hiyo pamoja na biashara husika kutoka BRELA.