Benki ya Azania yafungua tawi Dodoma

0
1912

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji amezitaka Benki nchini kushusha viwango vya riba za mikopo ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Dkt Kijaji ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua rasmi Benki ya Azania tawi la Sokoine na kusisitiza kuwa benki zina nafasi kubwa ya kuisaidia nchi kufikia azma yake ya kuwa ya viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kukuza mitaji ya wananchi.

Amesema kuwa hivi karibuni Serikali imechukua hatua madhubuti za kiutawala na kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo katika soko zinapungua.

Amezitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na serikali kuwa ni kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara, kushusha riba kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0 na kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0, hatua ambazo zimesaidia kupunguza riba katika soko kutoka wastani wa zaidi ya asilimia 20 hadi asilimia 17.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, – Charles Itembe amesema kuwa benki hiyo imeendelea kufanya vizuri katika soko kwa kupata faida na kwamba imejipanga kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wananchi mkoani Dodoma kwa viwango vya juu.