Athari na suluhisho la mdororo wa uchumi

0
553

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha akiwa ndiye mwendesha mjadala wa Mdororo wa Uchumi Ulimwenguni uliofanyika katika kituo cha kimataifa cha mikutano (JNICC) mkoani Dar es Salaam amesema sababu zilizopelekea kuwepo kwa mdororo wa uchumi ulimwenguni ni pamoja na athari zilizosababishwa na janga la UVIKO-19 kwa miaka michache iliyopita kutokana na watu kufungiwa ndani kwa baadhi ya nchi.

Amesema sababu nyingine za mdororo huo ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha ukame na mafuriko ya maji kwa baadhi ya nchi barani Afrika hali ambayo imeathiri uzalishaji mali.

Akieleza njia za kukabiliana na mdororo huo wa uchumi amesema upo umuhimu wa uzingatiaji wa uhakika wa chakula na uzingatiaji wa mnyororo wa thamani kwa bidhaa za chakula.

Maandalizi ya rasilimali watu ni jambo jingine la muhimu alilotaja akieleza kuwa moja ya sababu zilizochangia katika kukua kwa uchumi wa baadhi ya nchi za Asia ni kuwaandaa watu wa nchi hizo kufanya kazi katika viwanda kwa ubunifu na kwa tija.

Ameongeza kuwa kuibua fursa mbadala au kuzalisha bidhaa mbadala zitazoweza kukabiliana na mabadiliko ya soko badala ya kutegemea bidhaa aina moja ambayo kwa wakati fulani inaonekana kuwa ni changamoto sokoni.

Aidha, Dkt. Rioba amesema kuwa upo umuhimu wa kuiendeleza sekta ya huduma akitolea mfano Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inavyosisitiza umuhimu wa kuwekeza katika uchumi wa kidijitali ambapo ndipo dunia ilipojikita.

Kwa upande wa changamoto ambazo nchi zinapaswa kuzikabili ametaja kuwepo kwa siasa za kijiografia ambapo ulimwengu unakumbwa na migogoro ya vita vya mataifa makubwa pamoja na mwingiliano wa biashara kidunia.