Kampuni ya ndege Tanzania (ATCL) imesitisha safari zake za ndege kati ya Dar es salaam na Mumbai nchini India kuanzia hii leo, hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi imeeleza kuwa, safari hizo za ndege za kwenda Mumbai zimesitishwa kutokana na kuwepo kwa ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa corona nchini India.
ATCL imewataka abiria wote wenye tiketi za safari za kutoka Dar es salaam kwenda Mumbai kuwasiliana na ofisi za shirika hilo au mawakala wao kwa taratibu za kubadilisha tiketi, ili zitumike pindi safari zitakaporejeshwa tena bila gharama yoyote.
Kampuni ya ndege Tanzania imewaomba radhi wateja wake wote kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.