Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limeandaa safari kwa wafanyabiashara wazawa itakayofanyika Machi 4 mwaka huu kwenda Mumbai, India kwa ajili ya kukuza biashara baina ya Tanzania na nchi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano wa ATCL, Josephat Kagirwa amesema kuwa safari hiyo itahusisha wafanyabiashara na abiria wa kawaida na lengo lake ni kukuza biashara kwa wafanyabiashara wa Tanzania kwa kuwaunganisha na soko la India.
“Katika mkakati wa biashara wa ATCL ambao ulianza mwaka 2017 ambao utamalizika mwaka 2022, tumeandaa safari maalum kwa wafanyabiashara wazawa kwenda India kwa jukwaa la kibiashara la siku mbili kuanzaia Machi 5 hadi 6 mwaka huu, fursa ambayo itawasaidia wafanyabiashara kupata fursa masoko, kwani watatembelea maeneo mbalimbali ya biashara ikiwemo kituo maalum ambapo bidhaa zote duniani hufikia na kusambazwa,” amesema Kagirwa.
Tiketi kwa ajili ya safari hiyo maalum kwa Wafanyabiashara wa Tanzania kwenda nchini India zitapatikana kwa dola 500 za Kimarekani, ambazo zitahusisha kusafiri kwenda Mumbai na kurudi Dar es salaam pamoja na huduma za kutembelea masoko mbalimbali.