Wakunga na wauguzi wazembe walimwa adhabu

0
219

Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) ambalo ni mamlaka ya kisheria inayosimamia taaluma na wanataaluma wa Kada ya Uuguzi na Ukunga nchini, limewasimamisha kutoa huduma wauguzi na wakunga tisa huku wengine wanane wakipewa onyo.

Akizungumza na wanahabari Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Lilian Mselle, amebainisha kuwa, adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Uuuguzi na Ukunga na kanuni zake ya mwaka 2010, baada ya Baraza kuketi kwa siku mbili kusikiliza tuhuma zilizokuwa zikiwakabili wauguzi hao na wakunga kutoka mikoa mitano nchini.

Amesema wote waliopewa adhabu ya kusimamishwa au onyo ni kwa kushindwa kudumisha viwango vya taaluma na maadili.

Amesema, wauguzi na wakunga wawili kutoka kituo cha Afya Mikanjuni Jijini Tanga wamesimamishwa kutoa huduma kwa kipindi cha miaka 2 na mmoja mwaka 1. Kadhalika amesema wauguzi wanne wa kituo cha Afya Kibaoni Mjini Ifakara, wamepewa onyo.

Wengine waliokumbana na rungu la adhabu ni wauguzi wanne wa Hospitali ya Mji Geita ambapo mmoja amesimamishwa kutoa huduma kwa kipidi cha mwaka 1, wawili miezi sita na mmoja amepewa onyo.

Katika Kituo cha Afya Nyakumbu Kahama, wauguzi wawili wamesimamishwa kwa miezi sita na wawili wamepewa onyo. Halikadhalika, wauguzi wawili wa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga wamepewa onyo kwa kushindwa kudumisha viwango vya taaluma na maadili.

Prof. Mselle amefafanua kwamba adhabu zote zimetolewa kwa kuzingatia uzito wa kosa na ushiriki wa mhusika katika kosa husika.